Thursday, January 12, 2017

KILIMO CHA ZAO LA MGOMBA


Image result for mgomba
 

 

UTANGULIZI
Related imageHapa Tanzania kilimo cha migomba kimekuwepo Kwa miaka mingi.
Kilimo hiki ni maarufu sana kwa sababu zao la ndizi limekuwa likitumika
kama chakula kikuu kwa baadhi ya mikoa kama vile Kagera, Kilimanjaro
na Mbeya na hivyo kulifanya muhimu, kufuatia mazao ya mahindi,
mpunga, mtama, muhogo,viazi na mazao ya jamii ya kunde kama vile
maharage.
Zao la ndizi linaweza kuwa moja kati ya mazao ya biashara iwapo
litazalishwa kwa kufuata kanuni bora za uzalishaji wa zao hilo, ikwa ni
pamoja na kupanda aina bora ya migomba inayozaa ndizi
zinazotambulika katika masoko ya kimataifa.


ASILI YA MIGOMBA
Asili ya migomba ni nchi za Malaysia na India ambazo ziko Kusini
Mashariki mwa Asia. Migomba inayolimwa sasa imetokana na migomba
ijulikanayo kama Musa balbisiana ambayo asili yake ni India, na Musa
acuminata ambayo asili yake ni Malaysia.
Kutoka Malaysia na India migomba ilifika Afrika Mashariki katika karne
ya tano
MAENEO YANAYOLIMWA MIGOMBA NCHINI
Nchini Tanzania mikoa inayoshughulika na kilimo cha migomba na
kuzalisha zao la ndizi kwa wingi ni pamoja na Kagera, Kilimanjaro,
Mbeya, Arusha, Manyara, Mara, Tanga, Morogoro, Kigoma, na Pwani.
Hata hivyo zao hili linaendelea kuenea katika mkoa mingine nchini ikiwa
ni pamoja na Dar es salaam,, Mwanza, Ruvuma, Shinyanga na Lindi. Pia
Dodoma na Singida.
Kilimo cha migomba kinaweza kufanyika katika kipindi chote cha
mwaka kulingana na kiasi na mtawanyiko wa mvua hasa mabondeni au
kwa umwagiliaji.
MATUMIZI
Kilimo cha migomba kina faida nyingi, baadhi ya faida za migomba na
zao la ndizi ni: -
  •  Zao la chakula
  •  Zao la Biashara
  •  Kutengenezea pombe
  •  Kulisha mifugo
  •  Kutengenezea mbolea (mboji)
  •  Matandazwa shambani (mulch)
  •  Kutoa kivuli
UZALISHAJI
Zao la ndizi likizalishwa kwa utaalamu unaokubalika huweza kutoa
mazao yenye ubora wa hali ya juu na kuongeza uzalishaji kwa eneo.
Mambo yafuatayo yafaa kuzingatiwa katika uzalishaji wa zao hili.
(a) Hali ya hewa
Kiasi cha chini cha mvua kifaacho ni 100mm kwa mwezi au 1200mm
kwa mwaka.
Mwinuko ni kutoka usawa wa bahari hadi mita 1800 juu ya usawa wa
bahari. Zaidi ya mwinuko huo migomba haikui vizuri. Kiasi cha joto
kinachofaa ni nyuzi joto za sentigredi 25 hadi 30 chini ya nyuzi joto 16
migomba haikui vizuri.
Migomba hustawi vizuri kwenye udongo wenye rutuba ya kutosha, kina
kirefu, usiotuamisha maji na pia usiwe na chumvi. Chachu ya udongo
inafaa iwe kati ya pH 5 hadi 8.
(b) Aina za ndizi
Kuna aina nyigi sana za ndizi. Nchini Tanzania ndizi zinazozalishwa, zipo
za aina nyingi ambazo hutofautiana kwa majina kutokana na eneo au
mkoa unaozalisha. Hata hivyo zinaweza kugawanywa katika makundi
mawili. Aina ambayo huliwa kwa kuzichoma, kukaanga au kupikwa
zikichanganywa na vyakula vingine kama vile nyama. Aina za ndizi hizo
ni pamoja na Mzuzu, Mshare, Matoke, Bokoboko na Mkono wa Tembo.
Aina nyingine ni zile ambazo huliwa kama matunda, aina hizo ni kama
vile Kisukari, Kimalindi, Mzungu na Mtwike.
Kuna aina nyingine za ndizi ambazo kwa sasa huzalishwa hapa nchini
ambazo zina fahamika kwa ubora wake katika masoko ya ndizi ya
kimataifa. Aina hizi ni pamoja na Williams, Grand Naine, Pazz, Jamaica,
Gold Finger, Nyingine ni Uganda green, Embwailuma Giant na Chinese
Cavendish.
(c) Utayarishaji wa shamba
 Safisha sehemu inayohusika kwa kutumia zana ulizonazo.
 Ng’oa visiki vyote na mizizi yake yote
 Lima sehemu hiyo kwa kutumia jembe la mkono, rato, au trekta
ili kuwezesha mizizi laini ya migomba kupenya ardhini kwa urahisi.
 Baada ya visiki na magugu yote kuondolewa na hivyo ardhi
kuwa wazi, uchimbaji wa mashimo ya kupandikiza machipukizi                                                         au miche ya migomba unaweza kufanyika.
(d) Nafasi ya kuchimba mashimo
Mashimo yatachimbwa kwa nafasi inayokusudiwa kutumika kati ya
mashina ya migomba na kati ya mistari kama ifuatavyo:-
 Migomba inaweza kupandwa kwa nafasi ya Umbali wa meta
2.75 kwa 2.75 kwa migomba mifupi kama Kimalindi naKisukari. (Mashina 1,331 kwa hekta )
 Umbali wa meta 3 kwa meta 3 kwa migomba ya urefu wa kati
kama Jamaica na Mshare (Mashina 1,110 kwa hekta)
 Umbali wa meta 3.6 kwa meta 3.6 kwa migomba mirefu kama
Uganda green Mashina 760 kwa hekta).
(e) Uchimbaji mashimo. 
Uchimbaji mashimo inafaa ufanywe mapema kiasi cha juma moja hadimwezi kabla ya muda wa kupanda.Shimo lichimbwe kwa
kutenganisha udongo wa juu na wa chini.
Vipimo vya shimo ni vyema vikazingatiwa.
Iwapo utachimba shimo la mviringo litafaa liwe na kipenyo cha
sentimeta 60 hadi 90 na kina cha sentimeta 60 hadi 90. Iwapo
utachimba shimo la mstatili au mraba litakuwa na urefu, upana na
kina cha sentimeta 60 hadi 90, kutegemea kiasi cha mbolea
kilichopo na kiasi cha kvua kinachonyesha sehemu hiyo.
Uwekaji wa mbolea hufuatia mara baada ya mashimo kuwa tayari.
Kiasi cha madebe 5 ya mbolea ya samadi iliyooza vizuri au mboji
iwekwe kwenye lundo la udongo wa juu kando ya kila shimo na
ichanganywe kisha mchanganyiko wa mbolea na udongo
urudishiwe katika shimo kisha kijiti kichomekwe katikati ya shimo
hilo, ilikuonyesha sehemu ambapo mche au chipukizi litapandwa.
(f) Kuchagua machipukizi bora
Machipukizi mazuri yanayofaa kwa mbegu ni kama haya
yanayoonekana hapa chini: -
Sifa za chipukizi bora
  •  Liwe chipukizi sime, yaani lenye majani membamba na siyo
chipukizi maji yaani lisiwe lenye majani mapana.
  •  Litoke kwenye mgomba (shina) wenye afya nzuri, usiokuwa na magonjwa, minyoo ya mizizi, wala vifukusi vya migomba.
  •  Litoke kwenye mgomba wenye sifa ya kuzaa mikungu mikubwa.
  •  Liwe na afya nzuri na lisiwe na dalili za ugonjwa, wadudu, au mayai ya vifukusi.
  •  Urefu uwe kati ya meta 1 na meta 2 Kipenyo cha sehemu ya chini ya shina la chipukizi (tunguu) kiwe ni kati ya sentimeta 15 hadi 25.
(g) Upandaji wa machipukizi
  • Wakati unaofaa kupanda machipukizi ni mwanzoni mwa msimu wamvua.
  • Chomoa kile kijiti na chimba shimo la kiasi cha sentimeta 30x30 katikati ya shimo lililojazwa mchanganyiko wa udongo na samadikisha panda chipukizi hilo.
  • Rudishia udongo na hakikisha tunguu lote limefunikwa vizuri.
  • Shindilia udongo ili chipukizi lisimame wima imara.
  • Machipukizi yanayo tarajiwa kupandwa yanatakiwa kuondolewa mizizi yote ili kudhibiti minyoofundo na fukuzi wa migomba. Pia maji ya moto au dawa kama vile furadani inaweza kutumika.

UTUNZAJI WA SHAMBA NA MIMEA.
(a) Uwekaji wa matandazwa
Kazi hii ni vyema ikafanywa mara baada ya kupanda kama inawezekana.
Matandazo yawe ni makavu na unene wa sentimeta 15 ili kuhifadhi
unyevu, kuzuia magugu na yakioza yataongeza mbolea.
(b) Uongezaji wa mbolea
Baada kupanda ni vyema kuongeza mbolea madebe 2 kuzunguuka shina
la migomba kila baada ya miaka miwili au mitatu. Mbolea hii inatakiwa
kuchanganywa na udongo na kufunikwa kwa matandazwa.
(c) Umwagiliaji maji shambani
Migomba huhitaji maji mengi. Wakati wa kiangazi. Inafaa kumwagilia ili
kuto kupunguza sana ukubwa na wingi wa ndizi zinazotarajiwa kuvunwa
kwa mwaka. Kiasi cha maji kinachotakiwa kwa wiki ni milimita 25,
yaani eneo linalo zunguka shina la migomba lilowe kabisa.
(d) Kupunguzia machipukizi
Inatakiwa kupunguza mimea ya migomba kwa kila shina na kubaki
mimea mitatu tu, yaani Mgomba wenye ndizi (Mama), Mgomba
mkubwa ambao bado haujazaa lakini unakaribia kuchanua (Mtoto),
Mgomba mchanga uliochipua hivi karibuni ( Mjukuu)
(e) Uondoaji wa Majani Makavu
Mimea ya migomba inafaa iondolewe majani yote makavu ili kuondoa
uwezekano wa kuwepo mazalia ya wadudu na magonjwa, kuruhusu
mionzi ya jua na kufanya urahisi wa kuhudumia shamba .Pia hufanya
shamba kuonekana safi.
(f) Uondoaji wa ncha mwishoni mwa matunda
Baada ya mkungu kutoa ndizi, ua hunyauka na kubakiza ncha mwishoni
mwa matunda. Ncha hizo hupaswa kuondolewa .Huduma hii husaidia
kupunguza uwezekano wa kujeruhi matunda wakati wa kusafirisha
jambo ambalo kupunguza ubora wa tunda.
(g) Kuweka Miega
Miega ni nguzo au kamba ambazo hutumika kuzuia migomba iliyobeba
mikungu mikubwa isianguke kutokana na uzito mkubwa. Miega ni ya
lazima katika sehemu zenye upepo mkali. Kazi hii inatakiwa kufanywa
kwa uangalifu ili isijeruhi ndizi na mgomba wenyewe.
(h) Uondoaji wa kichombezo cha ua la kiume (Shumba)
Uondoaji wa shumba huwezesha matunda kukua vizuri, kuongezeka
uzito wa mkungu pia huzuia magonjwa kama vile ugonjwa wa mnyauko
wa migomba (Banana Baterial Wilt), ugonjwa wa Majivu nchani mwa
matunda (Cigar end rot). Ukataji hufanyika juu ya kovu la pili baada ya
kichana cha mwisho, kwa kutumia kisu kikali.
UVUNAJI
Zao la ndizi huweza kuanza kuvunwa katika kipindi cha miezi 9 hadi
miezi 15 tangu kupandwa kwa chipukizi. Muda wa kuvunwa hutegemea
hali ya hewa. Katika sehemu za joto ndizi huvunwa mapema zaidi kuliko
sehemu za baridi. Pia migomba iliyopandwa kwa kutumia machipukizi
huzaa mapema kuliko iliyopandwa miche iliyozalishwa kwa chupa
(tissue culture)
MATUMIZI YA RIBONI
Riboni za rangi moja (au alama ya kamba) hufungwa kwenye migomba
ya umri mmoja mara tu inapoanza kuchanua, na riboni ya rangi nyingine
hufungwa kwenye migomba itakayoanza kuchanua wiki mbili hivi
zinazofuata na kuendelea hivyo ili kurahisisha kuitambulisha mikungu
ambayo itavunwa kwa wakati mmoja. Pia matumizi ya riboni hurahisiha
utunzaji wa kumbukumbu ili kujua ni lini na ni mikungu mingapi
itavunwa.
WAKATI UNAOFAA KUVUNA
Mkungu wa ndizi huweza kuvunwa katika hatua tofauti kulingana na
matumizi, aina na mahitaji ya soko. Mkungu huachwa kwenye mgomba
mpaka vidole (matunda ) vimejaa. Uzito wa mkungu hongezeka haraka
katika wiki mbili za mwisho, ambapo migongo ya ndizi hutoweka.
Ndizi zinaweza kuvunwa zikiwa zimekomaa na zimeiva kwa kiasi cha
asilimia 75 kwa ajili ya kusafirishwa mbali, pia zinaweza kuvunwa zikiwa
kukomaa na zimeanza kuiva kwa ajili ya soko la karibu, au zikiwa
zimekomaa na kuiva kabisa kwa ajili ya soko na matumizi ya nyumbani
Njia bora ya kukata mkungu, ni ile inayohakikisha kuwa mkungu wa ndizi
hauanguki chini na kuvunja, kuchubuan au kuharibu ndizi, jambo ambalo
litapunguza ubora. Ukichelewa kuvuna ndizi zinaweza kuharibiwa na
ndege, wanyama, wadudu au kuibiwa.
UBORA WA NDIZI
Ndizi zenye sifa nzuri sokoni ni zile ambazo zimekomaa kwa kiasi
kinachotakiwa na zenye vidole vyenye urefu mzuri na visivyo na
michubuko. Pia ziwe hazijashambuliwa na magonjwa wala wadudu
waharibifu.
KIASI CHA MAVUNO
Mavuno ya ndizi hutegemea zaidi aina ya migomba, hali ya hewa,
utunzaji wa mimea shambani. Mavuno huweza kufikia hadi tani 60 au
zaidi kwa hekta kwa mwaka. Hata hivyo mavuno mazuri kwa mkulima
wa kawaida yasipungue kati ya tani 20 hadi 30 kwa hekta kwa mwaka.
MAGONJWA
Ugonjwa wa hatari sana ulioingia hivi karibuni katika wilaya ya Muleba
na maeneo mengine mkoani Kagera kutoka nchi jirani ya Uganda ni wa
Mnyauko wa migomba unaosababishwa na bakteria (Banana Bacterial
Wilt). Magonjwa mengine yanayosumbua zao hili ni Kuoza tunguu,
Ugonjwa wa panama, Ugonjwa wa majivu nchani mwa tunda, Sigatoka,
na Moko.
WADUDU WAHARIBIFU
Wadudu wanaosumbua zaidi hili ni Minyoo fundo (Banana nematodes),
na Vifukuzi (Banana weevils).
UDHIBITI WA MAGONJWA NA WADUDU WAHARIBIFU
Magonjwa na wadudu hawa huweza kuepukwa kwa kufuata kanuni bora
za uzalishaji wa zao hili. kama usafi wa shamba na kuchagua chipukizi
bora. Au kupanda miche iliyozalishwa kwa chupa (Tissue culture banana
seedlings) Hata hivyo mara mataizo haya yakitokea muone mtaalam wa
kilimo aliye karibu ili aweze kukupa ushauri.

No comments:

Post a Comment