Monday, June 4, 2018

Jinsi ya kutenganeza mbolea ya maji


Utangulizi
Mkulima anaweza kupunguza gharama, kuongeza rutuba kwenye udongo, mavuno pamoja na kipato kwa kutengeneza mbolea mwenyewe.
Mimea inaweza kukuonyesha inahitaji nini. Ni rahisi sana kugundua endapo mimea haipati virutubisho vya kutosha. Majani kubadili rangi ni ishara tosha kuwa mimea ina upungufu wa virutubisho. Ni lazima mkulima awe tayari kutatua tatizo hilo kwa haraka kabla hali haijawa mbaya. Upungufu wa madini ya nitrojen na fosiforasi ni jambo la kawaida kwa mimea. Virutubisho hivi vinahitajik kwa kiasi kikubwa sana kwenye mimea hasa katika hatua ya ukuaji.
Hata hivyo, ni muhimu kuelewa kwamba utatuzi unategemea hatua za kutunza udongo kwa kipindi chote cha mwaka. Lisha udongo ili ulishe mazao yako; tumia mboji, samadi, mbolea vunde, matandazo na utaratibu mzuri wa kupanda mazao kwa mzunguko.
Kunyunyizia kunafaa zaidi
Mkulima anaweza kusaidia hatua hii ya kulisha mimea inayokuwa kwa njia ya kunyunyizia mbolea ya maji. Kunyunyizia inasaidia kuipatia mimea virutubisho moja kwa moja kupitia kwenye majani na shina.
Unaweza kuona matokeo mazuri ya kuweka mbolea kwa kunyunyizia kulingana na kiwango cha mavuno, uwezo wa mimea kukabiliana na wadudu pamoja na magonjwa, kuvumilia ukame, na kuongeza ubora wa mazao. Mimea inakuwa na uwezo wa kunyonya mbolea mara 20 zaidi ya unapotumia aina nyinginezo za uwekaji wa mbolea kwenye mimea.
Kutengeneza mbolea ya maji
Aina hii ya mbolea hutengenezwa kwa kuchukua kiroba kilichojazwa samadi, aina mbalimbali ya mimea yenye virutubisho na inayoaminika kuwa dawa ya mimea. Kiroba hicho kinafungwa kwenye kijiti, na kutumbukiza kwa kuning’inia kwenye pipa lililojazwa maji. Kiroba hicho ni lazima kichukue kati ya kilo 30-50 za samadi pamoja na aina nyingine za mimea kwa maji lita 200 (tazama mchoro).
Mkulima anaweza kushika upande mmoja wa mti na kunyanyua na kushusha kila baada ya siku tano ili kuchanganya na kuharakisha kutolewa kwa virutubisho zaidi. Kwa kawaida mchanganyiko huo unakuwa na harufu kali sana maana Nitrojeni nyingi inayopatikana hugeuka kuwa Amonia. Ni vizuri kufunika pipa ili kuzuia kuyeyuka kwa nitrojeni. Harufu ikishaisha, ujue mbolea yako ipo tayari kwa matumizi. Ongeza maji na utingishe vizuri kabla ya kutumia. Nyunyizia mimea yako kila wiki mpaka utakapoona mabadiliko.
Tumia mimea peke yake
Kama unatengeneza mbolea ya maji kwa kutumia mimea peke yake, inashauriwa kutumia aina nyingi za mimea kama vile mivule, mibangi mwitu, majani ya minyanya, mwarobaini, mashona nguo, pamoja na vitunguu saumu. Aina hii ya mimea inasaidia sana katika kuzuia magonjwa, wadudu na kutoa virutubisho muhimu kwa mimea vinavyosaidia mkulima kupata mazao bora bila gharama ya ziada ya kununua virutubisho.
Vigezo vya kunyunyizia
Ili mbolea ya kunyunyizia iwe na matokeo mazuri, vigezo vifuatavyo vifuatwe:
• Inashauriwa kutumia mbolea iliyochanganywa vizuri ili kuepukana na kuunguza mimea.
• Acha maji utakayotumia kuchanganyia mbolea yako nje katika pipa lililowazi usiku kucha, hii inasaidia kutoa madini hatarishi, na kufanya mchanganyiko wenye faida kwa mimea.
• Tingisha vizuri. Chembechembe ndogo ambazo hazikuyeyuka zinaweza kuziba mdomo wa bomba la kunyunyizia.
• Matokeo mazuri yanaweza kupatikana endapo mbolea imechanganywa vizuri na kunyunyiziwa wakati hakuna upepo.
• Nyunyiza mbolea wakati wa asubuhi au jioni wakati hakuna joto na upepo ukiwa umepungua.

No comments:

Post a Comment